Onyo: Makala hii ina maelezo yanayoweza kuwasumbua baadhi

ya wasomaji. Polisi wa Afrika Kusini wamewakamata watu watano kwa tuhuma

za kuhusika na shambulio la kikatili dhidi ya mfugaji wa ng'ombe, Donovan

Marx, ambaye alipigwa na kuteswa katika tukio lililoelezwa kuwa la

"ukatili usio na maana". Marx, mwenye umri wa miaka 50, alishambuliwa wakati wa

uvamizi wa nyumba yake katika shamba lililoko Ventersdorp, mji mdogo katika

mkoa wa Northwest, Jumatano iliyopita. Kwa mujibu wa polisi, Marx alivamiwa alipokuwa akirejea

nyumbani, akapigwa risasi, kuchomwa kisu na kukatwa masikio katika tukio hilo

la kutisha. Washukiwa wote watano walikamatwa mwishoni mwa wiki, hatua

iliyopokelewa kwa furaha na mke pamoja na familia ya Marx, ambao walisema sasa

wanaamini mchakato wa sheria utachukua mkondo wake. Tukio hilo limezua hasira kubwa nchini Afrika Kusini, taifa

ambalo tayari linakabiliwa na viwango vya juu vya uhalifu wa kutumia nguvu. Shambulio lilivyotokea Polisi walisema kundi la watu waliovaa barakoa na wenye

silaha lilimvamia mfanyakazi wa shambani alipokuwa akikata nyasi katika eneo la

nyumba ya Marx. Washambuliaji hao walitaka kujua alipo Marx kabla ya

kumfunga mfanyakazi huyo mikono na miguu kwa kamba za plastiki. Marx aliporejea nyumbani, washukiwa wawili walimkaribia na

kumpiga risasi sehemu ya juu ya mwili. Baadaye walimvuta hadi ndani ya nyumba, wakamfunga mikono na

miguu na kudaiwa kumchoma kwa kisu mara kadhaa. Washambuliaji hao walivuruga nyumba wakitafuta mali na

kuondoka na bunduki tatu kutoka kwenye sanduku la kuhifadhia silaha, pamoja na

gari la Marx. Tukio hilo lilimalizika baada ya mfanyakazi aliyefungwa

kufanikiwa kujinasua na kuomba msaada. Marx alikimbizwa hospitalini ambako bado anaendelea kupatiwa

matibabu. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, huenda akahitaji

masikio ya bandia baada ya madaktari kushindwa kuyaokoa masikio yake ya asili. Viongozi walivyolaani tukio hilo Waziri wa Kilimo wa Afrika Kusini, Willie Aucamp,

alilaani shambulio hilo akisema hakuna nafasi nchini humo kwa vitendo vya

kikatili na visivyo na sababu kama hivyo. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Polisi, Ian

Cameron, aliwapongeza polisi kwa kufanya ukamataji wa haraka na kusisitiza

umuhimu wa uchunguzi wa kina ili kuhakikisha haki inatendeka. Washukiwa hao watano, wenye umri wa kati ya miaka 26 na 56,

wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne wakikabiliwa na mashtaka ya uvamizi

wa nyumba kwa kutumia silaha, jaribio la mauaji na kumiliki silaha pamoja na

risasi kinyume cha sheria. Mjadala kuhusu mashambulizi ya wakulima Baadhi ya makundi ya mrengo wa kulia yamekuwa yakitumia

mashambulizi dhidi ya wakulima weupe, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya

Waafrikaans, kudai kuwa kuna mauaji ya halaiki dhidi ya wazungu nchini Afrika

Kusini. Hata hivyo, madai hayo yamekataliwa na vyama vyote vya siasa

nchini humo, ikiwemo vile vinavyowakilisha jamii ya Waafrikaans. Takwimu za hivi karibuni za uhalifu nchini Afrika Kusini

zinaonyesha kuwa wahanga wengi wa uhalifu, ikiwemo kwenye mashamba, ni watu

weusi. Aidha, takwimu hizo hazionyeshi ongezeko maalum la mashambulizi dhidi ya

wakulima weupe.